BAJETI TEGEMEZI TANZANIA LAZIMA

Ninasikitishwa sana na utendaji wa wizara ya fedha katika suala zima la uandaaji wa bajeti kwa serikali ya Tanzania.
Kwasababu kila bajeti inaposomwa hakuna jipya katika kuongeza mapato kwaajili ya matumizi ya serikali katika suala lazima la kuboresha maisha ya watanzania zaidi ya kuwabana kwa kuongeza kodi katika bidhaa fulani;kwa mfano bajeti ya mwaka 2008/2009 wizara imeongeza kodi kwa 3% kwa makampuni ya simu vilevile kama kawaida yao katika vinywaji vyenye kilevi na visivyo na kilevi na sigara pia kuna ongezeko la kodi.
Ninachojua mimi hakuna ukomo katika ukusanyaji mapato bali kuna ukomo katika matumizi ya hayo mapato uliyokusanya.
Kwa hali hii inadhihirisha ni kwa kiasi gani Wizara ya fedha ilivyokuwa dhaifu katika suala zima la ubunifu wa vyanzo vingine vya mapato.
Binafsi sijaona sababu ya msingi ya kuongeza kodi kwa makampuni ya simu;inavyoeleweka mawasiliano ni kichecheo kikubwa cha ukuaji wa uchumi katika taifa lolote linalohitaji maendeleo ya kiuchumi;hivyo vinywaji na sigara kwa kiasi fulani ni sawa tu kwasababu ni anasa.Lakini kwa upande wa mawasiliano inashangaza,labda kwa mtizamo wa Wizara ya fedha ni anasa!
Kambi ya upinzani bungeni imeainisha vyanzo vya mapato 22 ambavyo Wizara ya fedha ingeweza kushughulika navyo na kuliongezea taifa mapato ambayo yangeweza kulipunguzia taifa kwa kiasi kikubwa katika utegemezi wa bajeti kutoka kwa wahisani hata kujitegemea kwa 100% katika bajeti kwa mapato yetu ya ndani ya nchi;na hata kuepuka utamaduni wa kila bajeti kuongeza kodi ya bidhaa fulani fulani.
Mfano wa hivyo vyanzo 22 vya mapato vilivyo ainishwa na kambi ya upinzani bungeni ni kama ifuatavyo:
Chanzo kikubwa ni madini,kilichoelezwa ni kwamba Wizara ya fedha na uchumi ilichotakiwa kufanya ni kushughulika na mapendekezo yaliyotolewa na kamati iliyoundwa na rais Jakaya Kikwete kuchunguza mikataba mibovu ya madini iliyosainiwa kipindi cha serikali ya awamu ya tatu;mojawapo ya mapendekezo ni mrahaba uongezwe kutoka 3% hadi 5%,misamaha ya kodi ifutwe na makampuni yaanze kulipa kodi mara moja kuchangia pato la taifa kama inavyofanyika kwa wawekezaji wengine.
Chanzo kingine ni mapato kutoka katika meli za uvuvi zinazofanya uvuvi katika maeneo yote ya Tanzania;kwasababu kilichogundulika hapa ni kwamba serikali inatumia gharama kukusanya mapato kwa wavuvi wadogowadogo na kuwaacha wavuvi wanaovua malaki hadi mamilioni ya samaki kila kukicha kinachotakiwa kufanya ni kujenga bandari za uvuvi.
Hata mimi binafsi nakiri udhaifu wa serikali katika ukusanyaji mapato,ni kweli wanatumia gharama na nguvu nyingi lakini mwisho wa mahesabu wananag’ang’ania kodi ya duka na muuza genge huku wakiacha kuchukua kodi kwa wawekezaji wa madini na mahoteli ya kitalii ukijumlisha na ubinafsishaji kwa taratibu mbovu zinazosababisha bei ya kutupa kwa rasilimali za taifa hili la Tanzania.
Sijawahi kusikia nchi ambayo inajiendesha kwa kutegemea tu kodi kutoka kwa wananchi wake na kuwasemehe kodi wawekezaji wa kigeni;kwa Tanzania kinachoonekana ni wananchi kuteseka ndani ya nchi yao na wageni kufurahia.
Swali la kujiuliza ni kweli tunaweza kuwa na bajeti inayotegemea mapato yetu kwa kutegemea kodi ya maduka na magenge yaliyopo nchini na kutoa msamaha wa kodi wa miaka kadhaa kwa wawekezaji wanaopata mapato ya mamilioni/mabilioni ya shilingi kwa siku kwa kigezo hiki cha tax holiday ambacho ni kwa wawekezaji wa kigeni pekee.Hivi ni kweli,mtanzania/watanzania akienda kuwekeza katika nchi za hao tunaowapa msamaha wa kodi(tax holiday),je na nchi zao zitatoa usamaria wa kutiana umaskini uliokithiri kama serikali ilivyofanya kwa kiasi kikubwa katika uongozi wa rais wa awamu ya tatu?
Jibu rahisi ni hakuna kitu kama hicho kwa nchi zilizoendelea hasa zinazotumia mfumo wa kibepari;na hata zilizokuwa katika mfumo wa ujamaa hakuna nchi itakayoingia kwenye mikataba mibovu kama ilivyojitokeza kwa Tanzania.Na kutengeneza sheria za kuwalinda wawekezaji wa kigeni na kuwabana wazawa,kwasababu ukweli uliopo ni kwamba wawekezaji wa kigeni ndiyo wanaofaidi msamaha wa kodi wa miaka mingi na siyo mtanzania.Hapa,pamoja na mambo mengine tunadhalilishana wenyewe kwa wenyewe huku mgeni akitushangaa na hatimaye kutudharau.
Kupitia hii mikataba mibovu na kuirekebisha yenyewe pamoja na sheria zake,hiki ni chanzo kingine cha mapato.Najua ni risk sana katika kuvunja mikataba lakini ukweli unabaki pale pale kwamba tunapoteza mapato mengi sana kwa hii mikataba mibovu ambayo inawanufaisha wageni ambao baadae wanaturudishia kilicho salia kwa njia ya misaada.Lakini,mjasiriamali mzuri ni yule anaye kubali kubeba risk(risk taker) kwasababu the higher the risk the higher the returns;hivyo basi itakuwa haina maana ya kuunda tume na kumtafuta mchawi ni nani.
Tanzania pamoja na ufisadi tumepewa misaada mingapi ya kifedha kutoka kwa nchi mbalimbali ambazo tunaziita wafadhili mara nyingine wahisani lakini mpaka leo hatuna maendeleo yeyote;na ninacho kifikiria hapa ni kwamba hii ni nuksi kwa viongozi wetu kukubaliana kama siyo kuhalalisha dhuluma hii kwa manufaa ya wageni na wao binafsi na ndiyo maana hata wakituletea hayo masalio bado hatuwezi kujikwamua katika lindi la umaskini uliokithiri.
Hivyo basi wizara ya fedha na uchumi kama kweli wanapenda kuwa na makusanyo ya mapato yasiyokuwa na kikomo walipaswa kulishughulikia hili.
Chaajabu,katika mapendekezo ya vyanzo vya mapato katika bajeti ya 2008/2009 Wizara ya fedha na uchumi imeendelea na utamaduni ule ule wa miaka yote wa kukaba kwenye kodi pamoja na hilo ilitakiwa kuwa na vyanzo vingine vya mapato pia kama vilivyotajwa na kambi ya upinzani bungeni.
Nchini Tanzania maamuzi mengi yanatolewa kwa mfano hili la kupandisha kodi linawanufaisha zaidi wafanyabiashara kuliko wananchi wengine.
Na hili linajitokeza katika mazingira yafuatayo,wafanyabiashara wanakuwa wanawahi kupandisha bei mapema zaidi hata kama anachouza kilikuwa katika stock;lakini likija suala la serikali kupunguza kodi/ushuru wafanyabiashara wanakuwa ni wagumu sana kushusha bei na mtumiaji wa mwisho ambaye ndiye mwathirika anapohoji ni kwanini inakuwa hivyo,majibu ya mara kwa mara ni kwamba hili ni soko huria,wanaotoa maamuzi hawana lolote la kutueleza wenyewe wanajilimbikizia fedha nyingi kwa maslahi yao binafsi,serikali(Tume ya bei) imekwenda likizo/mdebwedo.
Hivyo basi,kinachoonekana hapa kuna uozo katika utendaji wa serikali kwa kiasi cha watu kutokuwa na imani na serikali yao.Hapa serikali inatakiwa iwe makini katika yote yanayotolewa maamuzi kwa manufaa ya Taifa ni kimaanisha kuwe na ufuatiliaji wa makusudi kwa kila jambo lenye maslahi kwa Tanzania.
Kwa kuhitimisha Wizara ya fedha na uchumi kama itafuata mapendekezo yaliyotolewa na kambi ya upinzani bungeni,serikali itananufaika kwa haya yafuatayo:
Itaongeza mapato kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na miaka iliyopita,
Nidhamu na imani ya wananchi kwa nchi yao itakuwa juu(Uzalendo),
Tanzania na watu wake wataheshimika ndani na nje ya nchi,
Tutapiga hatua kiuchumi kuliko kisiasa kama viongozi wanavyotolea macho siasa zaidi kuliko uchumi.
Wizara ya fedha iwe na utaratibu wa kubuni vyanzo vingine vya mapato;ikiwezekana iombe msaada katika zoezi hilo kama wanaona ni gumu kwao pamoja na hayo bajeti ya mwaka wa fedha 2008/2009 imepitishwa tarehe 20/06/2008.
Tusiichukie Tanzania bali tuwachukie viongozi wake.

Advertisements

Acha maoni yako hapa

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s